Na Mwandishi wetu, Cologne Ujerumani
TANZANIA imeenfelea kunadi vivutio vya utalii katika nchi za Ulaya Magharibi ambapo wauzaji na wanunuzi katika sekta ya utalii wanakutana katika msafara huo wenye mawakala wa utalii zaidi ya 50.
Msafara huo unaojulikana kwa jina la _"My Tanzania Roadshow 2025" unaratibiwa na Kampuni ya Kili Fair unafanyika katika miji mitano ya Cologne Ujerumani, Antwerp Ubelgiji, Amsterdam Uholanzi, London na Manchester nchini Uingereza lengo likiwa ni kunadi vivutio vya Utalii vilivyopo Tanzania.
Akizungumzia Msafara huo Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania Ernest Mwamaja alisema kuwa wadau na wauzaji wa mazao ya utalii ukihusisha vyama vya waendesha utalii, wamiliki wa hoteli, makampuni ya ndege kutoka Tanzania wanakutana na wanunuzi wa utalii wa nchi hizo kwa ajili ya kufanya biashara.
Alisema nchi za ulaya ni soko kubwa linaloleta watalii wengi Tanzania ambapo Ujerumani pekee takribani watalii 100,000 wanatembelea vivutio vya utalii nchini kwa mwaka na kwamba kupitia misafara ya utalii huo muitikio wa wadau kushiriki umeendelea kuongezeka kila mwaka.
"Kupitia Misafara hii hasa katika soko la Ulaya Magharibi tutaendelea kuwashawishi wageni kuja Tanzania kwa wingi ili tuongeze pato la Taifa na tunaamini jitihada za kuboresha miundombinu ya utalii zinazoendelezwa". Alisema na kuongeza.
"Serikali ya awamu ya sita itachangia wageni wengi wanaokuja nchini na kukaa siku nyingi zaidi kwa kuwa tuna mtawanyiko wa vivutio vya utalii katika maeneo mengi".
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga akiilezea ongezeko la watalii kutoka nchi za Ulaya Magharibi alisema kuwa watalii 17,825 kutoka Ubelgiji wametembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania mwaka 2023.
Alieleza hayo wakati akizungumza na Wakala wa Utalii kutoka nchi ya Ubelgiji ambao wamekutana na Wakala wa Utalii kutoka Tanzania wakati wa msafara wa utangazaji u talii huo ujulikanao kama "My Tanzania Roadshow, Europe 2025"
Alisema kuwa idadi ya watalii kutoka Ubelgiji imeendelea kuongezeka hasa baada ya janga la Covid-19 ambapo mwaka 2020 watalii kutoka nchi hiyo walikuwa 5,364 pekee.
"Ongezeko hili linatokana na mikakati thabiti ya utangazaji inayoendeshwa na taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, na ushirikiano baina yao na ofisi yake idadi ya watalii imeongezeka kwa kasi na kufikia 17,825 mwaka 2023".alisema Balozi.
Alisema nchi ya Ubelgiji ni miongoni mwa nchi 15 zinazoleta wageni wengi zaidi Tanzania na kuongeza kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji utaendelea kutanganza vivutio hivyo kwa kufanya kazi kwa karibu na wakala wa utalii waliopo nchi za Ulaya.
Aliwataka wakala hao, mbali ya kushawishi watalii kutembelea Tanzania, wachangamkie fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii, na sekta nyingine za kiuchumi nchini.
Alibainisha kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara.
Aliipongeza Kampuni ya Kili Fair iliyoandaa Msafara huu, kwa kushirikiana na Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii za TTB, TANAPA, na NCAA.
Katika Msafara huo unaoshirikisha kampuni za sekta binafsi zaidi ya 50 unajumuisha pia taasisi za Serikali ambazo ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) na shirika za Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Ushiriki wa mashirika hayo unatoa hakikisho kwa sekta binafsi kuwa serikali inaunga mkono jitihada zao kwa kuweka mazingira rafiki, kuboresha miundombinu na huduma za utalii kwa wageni wanaotembelea Tanzania.