Na Said Njuki, Manyara Media Pro
TUZO mbili za kimataifa za World Travel zatua kibabe Chem Chem Safari lodge iliyopo wilaya ya Babati mkoani Manyara huku ikieleza siri ya kushinda tuzo mbili za kimataifa.
Tuzo hizo ni za hoteli bora ya kifahari Tanzania na hoteli bora ya kifahari Afrika, (luxury safari lodge Award) ambazo zilitolewa kwenye Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) zilizofanyika jijini Dar es Saalam hivi karibuni.
Ni mara ya kwanza kwa hafla ya tuzo hixo kufanyika Tanzania tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 na kushirikisha hifadhi za Taifa, Sekta mbalimbali za Utalii Duniani na Wawekezaji katika sekta hiyo.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari juzi mjini Babati, Mkuu wa Wilaya ya Babati Emmanuela Mtatifikolo na Meneja wa Huduma za hotel hiyo, Jorg Weytjens walisema siri kubwa ya ushindi huo unatokana na huduma bora upendo, nidhamu, kujituma na ushirikiano.
Mtatifikolo alisema Chemchem Safari Lodge ambayo ipo kati kati ya hifadhi za Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Manyara, katika eneo la Jumuiya ya hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge (Burunge WMA), imetunzwa katika mazingira ya asili kabisa na ukiwa ndani ya hoteli unashuhudia makundi ya wanyamapori kwa karibu zaidi.
“Licha ya kuwa na huduma nzuri na bora barani Afrika pamoja na uwekezaji bora uliofanywa na wamiliki wa hoteli hiyo chini ya Fabia Bausch na Nicolaus Negre ili kuvutia wageni lakini Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri ya kuwezesha watalii kuja Tanzania na kuitangaza vizuri Tanzania”. Alisema Mkuu wa Wilaya.
Alisema kwa wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara, chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga umeendelea kuweka mazingira bora ya kuendeleza Uhifadhi na Utalii ili kuvutia watalii kutembelea vivutio vilivyomo mkoani Manyara.
Alisema pamoja na hoteli Chem Chem kuendelea kufanya utalii wa picha katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wanyamapori, ziwa na vivutio kadhaa vya watalii, serikali kwa upande wake imeendelea kulitunza ikiwepo kudhibiti ujangili, uharibifu wa mazingira na kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi.
Kwa upande wake, Meneja wa huduma za hoteli hiyo Weytjens alisema siri nyingine ya ushindi ni huduma bora na ukarimu ambao wanapata wageni mashuhuri duniani wanaotembelea hoteli hiyo yenye hadhi ya kimataifa.
“Tunatoa huduma bora kabisa, wafanyakazi wanajituma sana kuwakarimu wageni lakini pia kuna ushirikiano mkubwa baina yetu kama hoteli, jamii inayozunguka hoteli, serikali ya Rais Samia Suluhu na wadau wengine”.alisema
Meneja wa Chem Chem lodge, Elizabeth Wambui alisema wamefurahi sana kupata tuzo hiyo kubwa mwaka huu, ambayo ni kati ya tuzo bora Afrika ambazo wamekuwa wakipata katika miaka ya karibuni.
“Tumefurahi kupata tuzo hizi, hii ilikuwa ni ndoto ya waanzilishi wa Chemchem Fabia na Nicolaus kutoa huduma bora kabisa Afrika na ndoto zao zimekuwa kweli”.Alisema
Alisema wafanyakazi wa hoteli, Serikali na jamii nzima ya Burunge wamekuwa na ushirikiano mkubwa ambao umekuwa ukichangia hoteli hiyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wageni.
Katika tuzo hizo mwaka huu Tanzania iliweka rekodi mpya kwa kushinda jumla ya tuzo 27 duniani, serikali ikinyakuwa tuzo 11 zikiwepo za vivutio bora vya utalii, bodi bora ya utalii, nchi bora ya utalii barani Afrika wa safari pamoja na viwanja vya ndege bora vikiwepo ya hifadhi za Taifa.
Sekta binafsi katika tuzo hizo, ilitwaa tuzo 16 zikiwepo za hoteli bora, kampuni bora za Utalii wa Safari,hoteli zenye huduma bora,hoteli zenye fukwe bora zinazovutia maelfu ya watalii duniani.
0 Comments