Na Catherine Mbena, Serengeti
MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Jenerali Mstaafu, George Waitara ameiagiza Menejimenti ya TANAPA kuhakikisha kuwa ujenzi wa daraja la Mto Kogatende unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili kuruhusu shughuli za uhifadhi na utalii kuendelea.
Jenerali Waitara alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki baada ya bodi hiyo kutembelea eneo la daraja hilo ambalo halipitiki hivi sasa, kutokana na uharibifu uliotokana na mvua kubwa zinazonyesha tangu mwaka 2020 na 2024.
“Ujenzi wa daraja ufanyike kwa wakati bila kikwazo chochote kwani ni muhimu sana kwa ustawi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kiutalii na kiuhifadhi...tunahitaji miundombinu imara katika hifadhi zetu ili shughuli za uhifadhi na utalii ziweze kuendelea vizuri". Alisema Jenerali Waitara na kuongeza.
"Ujenzi wa daraja hili ni suluhisho la kudumu la uhifadhi na utalii katika hifadhi ya Serengeti, hivyo Menejimenti ihakikishe mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili liweze kupitika kwa kipindi chote cha mwaka”.
Naye, Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya TANAPA, CPA Khadija Ramadhani, alishauri kuwa na daraja la juu kwa sababu kihisitoria inaonyesha daraja hilo awali lilikuwa na upana wa mita tano limeendelea kupanuka hadi kufikia mita 126.
"Gharama za upanuzi zimekuwa zikiongezeka kila wakati hivyo kuna haja ya kujenga daraja la kudumu ili kuepuka gharama za matengezo ya mara kwa mara kwa menejimenti". Alisema Khadija.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Stephano Msumi ambaye pia ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti alisema kuwa awali daraja hilo lilikuwa la boksi (vented drift) ambalo lilikuwa likitumika wakati wa kiangazi tu kutokana na kuwa la chini.
Alisema tayari uchambuzi yakinifu umeshafanyika ili kubainisha kina cha maji katika mto, hali ya udongo katika eneo la ujenzi wa daraja na historia ya ukubwa wa mafuriko katika mto huu kwa miaka 30 iliyopita ili kuja na usanifu wa michoro utakaokidhi viwango.
Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya hifadhi Nuhu Daniel alisema ukamilishaji wa usanifu wa kina na kuandaa michoro ya zabuni ili kuanza taratibu za manunuzi ya mkandarasi na ujenzi kuanza mara moja.
Alisema ujenzi wa daraja unakwenda kubadilisha kabisa uendeshaji wa utalii upande wa Kaskazini ambapo utalii utaweza kuendelea upande wa pili wa mto huo eneo la Lamai kiutalii hasa wakati msimu wa uvukaji wa nyumbu (Mara Crossing).
Mradi wa ujenzi wa daraja la Kogatende lenye urefu wa mita 100 unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ujerumani kupitia benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Gharama ya Euro milioni 2.2 sawa na kiasi cha takribani shilingi bilioni 6.3 na unatarajiwa kuanza mwezi Novemba mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati nchi yetu na Serikali ya Jamhuri ya Ujerumani.
Bodi pia ilitembelea miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Banagi - Lobo - lango la Kleins yenye urefu wa kilomita 72, barabara ya Golini - Naabi - Seronera yenye urefu wa kilomita 68.
Pia ilitembelea na ujenzi wa uwanja wa Golf “Serengeti National Park Golf Course” inayotekelezwa na kampuni tanzu ya TANAPA “TANAPA Investment Limited (TIL)” na ujenzi wa lango la Kleins unaotekelezwa na kampuni ya Stance Technic and Civil Engineers Limited.