Na Said Njuki, Arusha
MAMLAKA ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) imeapa kulinda rasilimali za asili na utamaduni wa hifadhi hiyo kwa kuhakikisha inabaki kuwa kivutio bora cha utalii duniani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo Dkt. Elirehema Doriye ya juzi imedai ulinzi wa rasilimali hizo na utamaduni wa asili utaendelea kuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
"Mamlaka itahakikisha Ngorongoro inabaki kuwa kivutio bora cha utalii duniani kwa kulinda rasilimali za asili na utamaduni kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho". Alisema Dkt. Doriye.
Alisema kila mmoja anajua katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, NCAA imefanikiwa kuboresha uhifadhi wa wanyamapori, kuongeza idadi ya watalii na mapato, kuboresha maisha ya wenyeji na kuboresha miundombinu ya utalii.
"Juhudi za kuhamisha wananchi kwa hiari, kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii zimeleta maendeleo makubwa katika hifadhi na Taifa kwa ujumla...hivyo hakuna sababu ya kutolinda rasilimali hizi".aliongeza.
Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo la kipekee duniani kwani lina hadhi tatu zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ambazo ni
Hifadhi ya Binadamu na Baiolojia, hadhi inayothibitisha umuhimu wa uhifadhi endelevu unaojumuisha binadamu na mazingira ya asili.
Urithi wa Dunia Mchanganyiko, inayotambua thamani ya kipekee ya maliasili na urithi wa kiutamaduni uliopo ndani ya eneo la hifadhi na Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark (Hifadhi ya Jiolojia ya Dunia), ambayo inahusisha mandhari ya kipekee ya kijiolojia, milima, volkano, na mabonde ambayo yanaelezea historia ya mabadiliko ya dunia.
"Mwaka 2023, Hifadhi ya Ngorongoro ilichaguliwa na Mtandao wa World Travel Awards kama Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (Africa’s Leading Tourist Attraction 2023). Hii ni heshima kubwa inayothibitisha umuhimu wa hifadhi hii katika utalii wa kimataifa".alisisitiza Dkt. Doriye.
Akizingumzia Uhifadhi na ulinzi wa rasilimali hizo Dkt. Doriye alisema katika kuhakikisha uhifadhi bora wa rasilimali za hifadhi, NCAA imefanikiwa kutekeleza hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudumisha hadhi za Kimataifa.
Alisema Mamlaka imeendelea kuhakikisha
eneo hilo linaendelea kuwa moja ya maajabu saba ya asili barani Afrika, likiwa na miamba na sura za nchi zinazoelezea historia ya dunia na uumbaji wake.
"NCAA imeendelea kudhibiti mimea vamizi katika eneo la zaidi ya hekta 5,207.5 ndani ya hifadhi...hatua iliyoboresha uhifadhi wa wanyamapori na ikolojia yao huku mfumo wa ufuatiliaji wa wanyamapori ukiimarishwa ambapo faru 29 wamewekewa alama za masikio na vinasa mawimbi kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wao". alisema.
Kuhusu ujangili alisema NCAA, kwa kushirikiana na vikosi maalum na vyombo vya usalama, imefanikiwa kudhibiti ujangili wa wanyamapori ndani na nje ya Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Pololeti.
Alisema matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kutoka 25 mwaka 2020/2021 hadi tukio moja tu mwaka 2022/2023, na hakuna tukio lolote mwaka 2024 huku wakikamata watuhumiwa 207 wa ujangili, ambapo 175 wamefikishwa mahakamani.
"Mitandao ya ujangili inayotumia sumu na silaha za jadi imevunjwa katika maeneo mbalimbali...mafanikio haya yanatokana na ushirikiano madhubuti na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kulinda wanyamapori".alisema.