Kamishna Kuji awafunda Wakuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania

 





Na Andrew  Mbai,  Dodoma

KAMISHNA wa Uhifadhi Musa Juma Kuji amewafunda Wakuu wa Hifadhi za Taifa katika kikao kazi kilicholenga kufanya tathmini ya hali ya uhifadhi na utalii jijini Dodoma jana.

Kikao hicho pia kilipokea ushauri na maoni ya namna bora ya kuboresha utendaji kazi katika hifadhi za Taifa ili kuhakikisha hifadhi hizo zinakuwa endelevu.

Aliwataka wakuu wa hifadhi hizo kuongeza jitihada katika utendaji kazi ili kuboresha ukuaji wa utalii pamoja na kuongeza mapato kwa Taifa.

“Tuendelee kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa tunabuni mazao mapya ya utalii ambayo yatakuwa na matokeo ya kuongeza mapato ndani ya shirika na serikali kwa ujumla". Alisema na kuongeza.

"Nakubaliana na ushauri wenu wa kuongeza nguvu ya kuyafikia masoko ambayo yanaongoza kuleta watalii wengi wanaotembelea hifadhi zetu".

Wakuu hao walimpongeza Kamishna Kuji kwa namna anavyoendelea kujitoa na kuwafikia maafisa na askari wa uhifadhi katika maeneo yao ya kazi kwa kufanya nao vikao, kuwasikiliza na kuwatia moyo jambo ambalo limekuwa likileta tija kwa watumishi na kuwaongezea morali ya kazi.

“Afande Kamishna tunakushukuru na kukupongeza sana kwa uamuzi wako wa kufanya ziara za kutembelea hifadhi na kukutana na maafisa na askari katika vituo vyao kwani jambo hilo limesaidia sana kutatua changamoto zilizopo...hivyo watumishi wamekuwa wakipata faraja na kuongeza morali ya utendaji kazi, hongera sana afande”. alisema Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Charles Ngendo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe.

Aidha, Wakuu wa hifadhi hao walipata fursa ya kujadili masuala muhimu ambayo yamelenga kuboresha utendaji kazi pamoja na kuinua kiwango cha utoaji huduma kwa watalii wanaotembelea hifadhi za Taifa Tanzania.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linasimamia jumla ya hifadhi 21 ambazo kila hifadhi ina Mkuu wa hifadhi ambaye ni Afisa wa cheo cha juu cha maamuzi ya mwisho kwa ngazi ya hifadhi husika na ni kiungo muhimu  katika usimamizi na uratibu wa shughuli za uhifadhi na utalii nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post
NJUKI MEDIA