Imarisheni Uhifadhi na Utalii Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato

 




Na Philipo Hassan, Burigi - Chato

KAMISHNA wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Nassoro Kuji, amewataka maafisa na askari wa hifadhi ya Taifa Burigi - Chato, kuwajibika kikamilifu katika kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii.

Kuji alisema hayo juzi alipofanya ziara ya kikazi katika hifadhi hiyo kwa lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na utalii ambapo alipokelewa na Kamanda wa uhifadhi Kanda ya Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Izumbe Mgana Msindai na Kamishna Msaidizi wa uhifadhi Simon Aweda  ambaye pia ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato.

“Ongezeni ubunifu katika utendaji kazi ili kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii  na kuongeza idadi ya watalii na mapato kufikia azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania". Alisema CC Kuji.

"Lengo ni kufikisha idadi ya watalii milioni tano na mapato ya dola bilioni 6 za kimarekani kwa mwaka wa fedha mwaka 2025”.aliongeza Kamishna Kuji.

Aidha, Kamishna Kuji alisisitiza kutumia rasilimali watu vizuri pamoja na kuruhusu ubunifu wenye tija katika utendaji kazi ili kuleta matokeo chanya.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Simon Aweda alimshukuru Kamishna Kuji  kwa kutenga muda wake na kukutana  na watumishi.

Alieleza kuwa hifadhi inaendelea na mikakati ya kuboresha miundombinu ya utalii na kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama ikizingatiwa kuwa hifadhi hiyo inapakana na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.

“Hifadhi yetu inazidi kuimarika kiusalama na ina nafasi kubwa ya kukua kiutalii kwani kuna fursa mbalimbali za uwekezaji wa kambi za watalii na hoteli hivyo tunaendelea kutangaza fursa hizi ili kuongeza mapato ya serikali na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa”. aliongeza Kamishna Aweda.

Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato iliyopo Kanda ya Magharibi  ni maarufu kwa wanyama adimu aina ya Mbega Wekundu (Ashy Red Colobus Monkey).

Post a Comment

Previous Post Next Post
NJUKI MEDIA